Skip to content


Matumizi mabaya ya mtandaoni yanaleta taharuki ya dharura na linalokua kutishia uhuru wa kujieleza, usawa na ujumuishi.

Iwe unapitia au unashuhudia unyanyasaji mtandaoni, Mwongozo huu wa mafunzo unatoa mikakati madhubuti ya jinsi ya kujitetea mwenyewe na wengine. Tuliandika mwongozo huu kwa ajili ya wale ambao wameathiriwa kupita kiasi na matumizi mabaya ya mtandaoni: waandishi wa habari, wanaharakati na wasanii wanaojitabulisha kama wanawake. Bila kujali utambulisho au taaluma yako, mtu yeyote anayefanya kazi mtandaoni atapata zana na nyenzo muhimu hapa za kuelekeza matumizi mabaya ya mtandaoni na kuimarisha usalama wa kidijitali.

Kuhusu Mwongozo huu

Matumizi mabaya ya mtandaoni ni tishio la moja kwa moja kwa uhuru wa kujieleza na yanaweza kuwa na athari mbaya kwa tija yako, hali nzuri ya mwili na afya ya akili. Iwapo unakabiliwa na matumizi mabaya ya mtandaoni, Mwongozo huu wa Mafunzo unatoa mikakati na nyenzo za jinsi ya kujilinda, kujibu na kusaidia wengine.

Mwongozo huu uliundwa na wale ambao wanalengwa kwa taaluma na utambulisho wao: waandishi wa habari, waandishi, na wanaharakati, wakiwemo wanawake na wale walio katika makundi yaliyotengwa. Tunatumai mwongozo huo utasaidia kwa mtu yeyote anayepata matumizi mabaya ya mtandaoni.

Mwongozo huu ambao uliundwa kwa Kiingereza mwaka wa 2018 kwa ajili ya hadhira ya Marekani, umebadilishwa na kutafsiriwa hadi Kiswahili na wanahabari, watafiti na wanaharakati wa haki za kidijitali walio nchini Kenya na Tanzania. Lengo letu ni kushughulikia vyema mahitaji ya wanahabari, waandishi na wanaharakati katika Afrika Mashariki, ambao wanazidi kunyanyaswa mtandaoni ili kupata haki ya kazi zao. Takriban wanahabari saba kati ya wanawake kumi nchini Kenya wamenyanyaswa mtandaoni wakiendelea na kazi zao, kulingana na utafiti wa 2019 uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake nchini Kenya (AMWIK) na Article 19 Eastern Africa.

Kuhusu waandishi

Mwongozo huu ulirekebishwa kwa muktadha wa Afrika Mashariki na Cecilia Mwende Maundu. Maundu ni mwandishi wa habari wa utangazaji, mtafiti wa haki za kidijitali, na mtaalamu wa usalama wa kidijitali anayefanya kazi katika makutano ya uandishi wa habari, teknolojia, na utawala wa mtandao. Anaendesha mafunzo ya usalama wa kidijitali katika bara zima la Afrika kwa wanahabari wanawake na vikundi vingine vya watu wachache na pia ndiye mwanzilishi wa “Digital Dada,” podikasti iliyolenga kuwawezesha wanahabari wanawake ambao wamekumbana na unyanyasaji mtandaoni na kuchukua hatua za kujilinda na kupigana.

Bonface Witaba na Peter Mmbando yaliyotafsiriwa kwa Kiswahili. Witaba ni mwandishi wa Kenya, mshairi, mkufunzi wa haki za kidijitali, na mtafiti wa utawala na sera wa mtandao aliyeko nchini Kenya. Mmbando ndiye mwanzilishi mwenza na mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la serikali Digital Agenda for Tanzania Initiative. Mmbando anatetea utawala wa mtandao, haki za kidijitali na sera za ujumuishaji za kidijitali. Pia ni mkufunzi, mwanaisimu na mwandishi wa utafiti ambaye anachangia maendeleo ya sera kupitia michakato ya wadau wengi.  

Lucy Kilalo alihariri yaliyomo kwa Kiswahili. Yeye ni mhariri mwandamizi wa Taifa Leo Newspaper, chapisho la Nation Media Group, chombo pekee cha habari kwa Kiswahili nchini Kenya.

Tunamshukuru Tawanda Mugari, mwanzilishi mwenza na mkuu wa kitengo cha teknolojia katika Digital Society of Africa, na kwa waandishi wa habari na wataalamu wote walioshiriki uzoefu na utaalamu wao katika uundaji wa mwongozo huu kwa Kiswahili.